Kenya inaweza kujifunza nini kwa mfumo wa uongozi wa Rwanda?

g

Chanzo cha picha, Olivier Mugwiza/ The new times Frickr

Maelezo ya picha, Rais wa Rwanda Paul Kagame akizungumza na wakazi katika mkutano wa hadhara wa wilaya ya Nyamagabe kusini mwa Rwanda
  • Author, Dinah Gahamanyi
  • Nafasi, BBC Swahili News
  • Akiripoti kutoka Nairobi

Nchini Rwanda sasa umekuwa ni utamaduni wa kawaida kwa Rais kuwatembelea wananchi katika wilaya zao na kufanya mikutano ya ana kwa ana na wananchi ili kuwasikiliza na kuwashirikisha katika juhudi za kuboresha huduma za kiserikali zinazotolewa kwao.

Baada ya vikao hivyo rais hufanya vikao vya faragha na viongozi wa kijamii (opinion leaders) wakiwemo viongozi wa dini na kijamii wa kikanda.

Mikutano hii ni wakati pia wa rais kuelewa matatizo mbali mbali hususan ya kijamii yanayowakabili wananchi na kuyatafutia suluhu hapo hapo au baadaye. Katika mikutano ya aina hii ya hadhara rais huwasikiliza raia mmoja baada ya mwingine huku wakitoa kero zao na kuzipatia suluhu za moja kwa moja.

g

Chanzo cha picha, Olivier Mugwiza/ The new times Frickr

Maelezo ya picha, Rais Kagame akizungumza katika mkutano wa mazungumzo ya ana kwa ana ya kitaifa yanayofahamika kama Umushyikirano

Mazungumzo ya ana kwa ana ya kitaifa yanayofahamika kama Umushyikirano pia hufanyika mwezi Disemba kila mwaka ambapo rais binafsi huwaalika Wanyarwanda wanaoishi katika nchi za kigeni pamoja na wale wanaoishi ndani ya nchi kuzungumzia masuala muhimu ya yanayozunguka sera za kukuza umoja, maridhiano na maendeleo ya nchi.

Je Kenya inaweza kujifunza nini kutokana na mazungumzo ya ana kwa ana na raia?

g

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Maandamano nchini Kenya yalisababisha umwagaji damu

Hivi karibuni nchini Kenya kumeshuhudiwa kuibuka kwa upinzani kwenye mitandao ya kijamii na mitaani vijana wanaojiita Gen-Z wanapaza sauti dhidi ya serikali ya Rais William Ruto kutokana na kile wanaocheeleza kuwa rais na serikali yake wameshindwa kuwasikiliza wananchi hivyo kuamua kujichukulia maamuzi wenyewe kuhusu masuala yanayowahusu wananchi, bila kuwashirikisha wananchi.

Makumi ya watu waliripotiwa kuuawa huku wengine kwa mamia kujeruhiwa kufuatia maandamano hayo.

Kufuatia maandamano, Rais William Ruto alichukua hatua ya kuwaalika vijana vijana wenye hasira katika mazungumzo ya moja kwa moja kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kupitia Twitter Space kusikiliza maoni yao.

Hatua hii kwa kiwango fulani imeonekana kuwa nzuri kwa baadhi ya Wakenya kuelekea uwajibikaji wa serikali ya Rais Ruto, huku wengine wakiiona kuwa haitoshi kwa sasa kutatua kero za wananchi.

‘’Inaelekea ni kama sasa amegundua kuwa kukaa Ikulu na kuongea tu haitamsaidia hivyo ilibidi awafuate vijana twitter. Kwa maoni yangu hiyo ni hatua nzuri kama akiendelea hivyo,’’ anasema Muthoni Grace mkazi wa Nairobi.

Kinyume na Muthoni, Karanja George mwanafunzi wa chuo Kikuu hajaridhika na mazungumzo ya Rais Ruto na vijana kupitia mtandao wa X: ‘’My Space ni yetu sisi vijana, rais anakuja kufanya nini?, ni sisi tuliokuwa tumeanza kuzungumza shida zetu na kusema aondoke madarakani…aliiteka’’, alisema George na kuongeza: ‘’Yeye anafaa kutufuata kule tuliko, kuna shule, kuna maeneo wanakuwa, tuongee naye tukimuona, mbona ajificha kwa Twitter?.’’, alisema.

g

Chanzo cha picha, Olivier Mugwiza/ The new times Frickr

Maelezo ya picha, Katika mikutano ya hadhara ya ana kwa ana na Rais Kagame, mkazi wa wilaya ya Nyamagabe Kusini mwa Rwanda akimueleza rais jambo
w

Chanzo cha picha, Olivier Mugwiza/ The new times Frickr

Maelezo ya picha, Katika mikutano ya ana kwa ana, rais na viongozi wa kikanda na kimataifa wa njanja mbali mbali hupata fursa ya kuuliza maswali kwa viongozi kuhusiana na masuala mbali mbali ya kibinafsi na kijamii

‘’Nafikiri kuna somo ambalo rais wa Kenya anaweza kujifunza kutoka kwa mwenzake wa Rwanda, anasema Noel Rutikanga, Mhadhiri na Mwanahistoria, kutoka Chuo Kikuu cha Rwanda (UNR).

‘’Rais wa Rwanda amekuwa akiwafuata wananchi na kuwasikiliza binafsi na kuelewa mahitaji yao, kuanzia mashinani hadi ngazi ya kitaifa na kuhakikisha kuwa matakwa yao yanatekelezwa…amekuwa akizungumza na makundi mbali mbali ya vijana, mashirika ya watu wenye ulemavu na wote wanaripoti kwake juu ya kile kinachotokea, kumueleza matarajio yao, namna yanavyotimizwa na matatizo waliyo nayo na kisha kutoa mchango wao kuhusu namna yanavyoweza kutatuliwa ,’’ anasema Noel Rutikanga ambaye amekuwa akifuatilia matukio ya hivi karibuni ya vugugugu la vijana wa Gen-Z nchini Kenya.

Aliongeza: ‘’Katika kuhakikisha mikutano yake inatekelezwa rais huwaagiza viongozi kuanzia mashinani kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji, tathmini na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike, kuhusu matatizo yaliyojitokeza, na jinsi utekelezaji unavyofanyika.’

Kando na maagizo hayo kila kiongozi katika ngazi zote za kitaifa kwa ushirikiano na raia, hutakiwa kujiwekea malengo ya utendaji na kipimo cha mafanikio (au Imihigo) kwa kipindi fulani, ambayo huwajibishwa na raia, pale anaposhindwa kuyatekeleza. Baadhi ya viongozi wanaposhindwa kutekeleza malengo hayo hulazimika kujiuzuru ili kutoa fursa kwa mtu mwezi uwezo kuhudumu.

g

Chanzo cha picha, Goverment of Rwanda

Maelezo ya picha, Katika mojawapo ya mikutano ya faragha viongozi wa ngazi na sekta mbali mbali kuanzia ngazi za mwanzo hadi ngazi ya kitaifa kutathmini utendaji na utoaji huduma bora kwa raia.

Mbali na Umushyikirano, rais pia viongozi wa ngazi mbali mbali za kitaifa za uongozi huitisha vikao katika nyakati tofauti za mwaka vinavyofahamika kama Umwiherero (kikao cha faragha) vinavyowajumisha viongozi wa ngazi na sekta mbali mbali kuanzia ngazi za mwanzo hadi ngazi ya kitaifa kutathmini utendaji wao na mafanikio huku wakiweka mikakati ya utendaji wa kipindi kinachofuata.

‘’Kwa mtindo wa utendaji wa uongozi wa rais na viongozi kuwasiliana na raia ana kwa ana, maandamano kama yaliyotokea Kenya hivi karibuni sidhani kama yanaweza kutokea Rwanda’’ anasisistiza Bw. Rutikanga.

Ziara zinazowatia ‘’tumbo joto’’ viongozi

g

Chanzo cha picha, Olivier Mugwiza/ The new times Frickr

Maelezo ya picha, Mmoja wa viongozi wa kikanda akijibu maswali ya rais na raia. Katika mikutano ya ana kwa ana , baadhi ya viongozi hukabiliwa mtihani wa kujibu baadhi ya maswali ya wananchi, na baadhi yao hulazimika kujiuzuru

Mara nyingi maeneo yanayotembelewa na Rais Paul Kagame kwa ajili ya mikutano hiyo hufahamishwa kwa kipindi kifupi kabla ya kutembelewa na mkuu wa nchi.

Rais Kagame huketi katika viwanja vya umma, mathalani katika viwanja vya michezo huku raia wakijipanga misururu mirefu mbele yake na kupewa kipaza sauti kuelezea kero na dukuduku na mara nyingine shukran zao kuhusiana na huduma za serikali katika maeneo yao na uongozi kwa ujumla.

Katika mkutano huu Rais Kagame hupata fursa ya kuyasikiliza na kujibu baadhi ya maswali kutoka kwa mwananchi, na yale yanayowahusu viongozi wa kieneo au mawaziri husika na kero zilizotolewa hupata suluhu kwa wananchi.

Si ziara zinazofurahisha kwa baadhi ya viongozi ambao huwa wamelegea kazini na kushindwa kuwajibika ipasavyo kutekeleza majukumu kwa raia. Baadhi hujikuta wakizongwa kwa maswali ya raia na rais na pale wanapobainika kushindwa kabisa kuwajibika katika utekelezaji majukumu yao hulazimika kujiuzulu.

Mazungumzo ya mikutano hii hupeperushwa moja kwa moja kupitia radio na televisheni ya taifa, na mitandao ya kijamii hivyo hufuatiliwa na umma Wanyarwanda ndani na nje ya nchi.

‘’Ni dhahiri kwamba Rwanda na Kenya ni nchi mbili zenye historia na mfumo tofauti wa uongozi, lakini bila shaka kuna mambo ambayo Kenya inaweza kujifunza kutoka kwa Rwanda hususan umuhimu wa mkuu wa nchi kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ya ana kwa ana na raia ili kuyatafutia ufumbuzi matatizo kwa pamoja na raia’’, anahitimisha Bw Rutikanga.

Unaweza pia kusoma:

Imeandikwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Florian Kaijage