Kwa nini Wakenya bado wanaandamana?

Mwandamanaji

Chanzo cha picha, Peter Njoroge/BBC

Wakenya bado wanakadiria matokeo ya maandamano ya wiki mbili zilizopita ya kupinga nyongeza ya kodi, ambayo yalisababisha watu kupoteza maisha, kujeruhiwa, na wengine kukamatwa kwa uharibifu mkubwa wa mali.

Idadi ya waliofariki kutokana na maandamano hayo imefikia 39, huku 361 wakijeruhiwa, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu Kenya. Serikali haijathibitisha takwimu hizo.

Rais William Ruto ameahidi kuliondoa jeshi barabarani iwapo maandamano hayo yatakuwa ya amani.

Maandamano hayo yalianza kama malalamiko ya mtandaoni kuhusu nyongeza ya kodi ya karibu dola bilioni 2.7 katika pendekezo la muswada wa fedha wa 2024, yamegeuka vuguvugu la kitaifa la kupinga ufisadi na utawala mbaya.

Rais Ruto amejitolea kufanya mazungumzo na vijana na ameahidi kupunguzwa kwa bajeti ya usafiri na katika ofisi yake kulingana na matakwa ya baadhi ya waandamanaji.

Wanachama wa vuguvugu la vijana wasio na viongozi wamesema hawana imani na rais kutekeleza mipango yake mipya ya kubana matumizi.

Soma pia:

Kugeuka kwa sura ya maandamano

Maandamano hayo ambayo sasa yameingia wiki ya tatu yalianza kwa kupinga muswada tata wa fedha uliokuwa unapendekeza nyongeza ya ushuru na ambao hatimaye rais William Ruto hatimaye aliutupilia mbali kufuatia shinikizo la umma,

Lakini maandamano hayo sasa yamechukuwa sura mpya ambapo raia wanashinikiza rais kujiuzulu pamoja na kulaumu serikali kwa mauaji ya waandamanaji kadhaa wiki iliyopita.

Katikati ya mji mkuu wa Nairobi biashara zilifungwa huku polisi wakikabiliana na waandamanaji. Maandamano pia yamefanyika katika mji wa pwani wa Mombasa na Kisumu magharibi mwa Kenya.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwemo Tume ya Haki za kibinadamu nchini Kenya(KNCHR) yanasema tangu maandamano ya kupinga muswada wa fedha kuanza wiki mbili zilizopita takribani watu 39 wameuawa na vikosi vya usalama.

Baadhi ya waandamanaji waliozungumza na BBC wanasema licha ya ya kwamba muswada wa fedha wa mwaka 2024 kutupiliwa mbali na rais, bado mambo hayajakaa sawa na wanataka masuala muhimu kama vile kupanda kwa gharama ya maisha yashughulikiwe.

''Tumechoka na ufisadi wa serikali hii, tumechoka na uporaji na ubadhirifu wa mali katika serikali hii,'' alisema Kasamuel Mc Oure mmoja wa vijana wanaongoza maandamano hayo jijini Nairobi.

Oure anaongeza kuwa wamerejea tena kwa maandamano kwa sababu wamechoshwa na ''mauaji ya vijana wenzao.''

Mjini Mombasa pwani ya Kenya mwandamanaji mmoja alisema,‘’Tumekuja kupigania haki yetu. Tumenyanyaswa ya kutosha. Vitu tulivyoahidiwa na serikali havijatimizwa mpaka sasa.’’

Viwango vya ukosefu wa ajira vinaendelea kuongezeka, huku gharama ya maisha ikizidi kupanda kila uchao. Kutokana na hali hii ya kuvunja moyo sasa baadhi ya Wakenya waliochukizwa na hali yao ya maisha wamegeukia mitandao ya kijamii kuangazia hali ya maisha ya viongizi na wandani wa karibu wa rais - jinsi ''wanavyoponda raha.''

Vijana

Chanzo cha picha, Reuters

Kumekuwa na taarifa kwamba baadhi ya watu wanatumia maanamo hayo kuvamia biashara za watu.

Siku ya Jumatano Waziri Serikali ya Kenya imesema wahuni wote waliohusika katika uporaji na uvunjaji wa sheria katika miji ya Nairobi na Mombaswa watachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Katika taarifa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Profesa Kindiki Kithure amesema kuwa kuna ripoti makundi hayo ya wahuni yanapanga kuendeleza uhalifu na uporaji wa mali Alhamisi wiki hii na kusema kwamba serikali haitaruhusu hilo kutokea.

''Baada ya kukamilika kwa uchunguzi unaoendelea, serikali inawahakikishia wananchi wapangaji, watekelezaji na wafadhili wa uchomaji moto mkubwa, ujambazi wa kutumia nguvu na makosa mengine ya uhalifu watafikishwa mahakamani,’’ alisema Kindiki.

Waandamanaji wanataka nini?

Swali ambalo wwengi wanajiuliza ni kwa nini bado maandamano yanaendelea licha ya Rais William Ruto kuutupilia mbali ule muswada tata wa fedha?

Mtaalamu wa uongozi bora Stella Agara, anasema vijana ambao waliandamana kupinga muswada wa fedha hawajaridhika na majibu ya rais ingawa walifurahia kwamba alikataa kuutia saini wanahisi hajatilia maanani mchango wao katika jamii.

Katika hotuba yake kwa taifa Alhamisi wiki iliyopita Rais William Ruto aliwataja vijana hao kuwa wahalifu, jambo ambalo liliwaghadhabisha sana.

Bi Agara aidha anasema jambo lingine linalochochea maandamano haya mapya ni kwamba vijana walioshiriki maandamano ya wiki iliyopita wanahisi wahalifu wanatumiwa kusambaratisha maandamano yao. ''Wanaona mwenendo huo unarudisha nyuma juhudi walizopiga katika maandamano yao ya awali kwa sababu ya watu hao walioletwa kupora na kuharibu miundo mbinu ya serikali.''

Kuhusuana na suala la Rais Ruto kuahidi kuongea na vijana hao wa Gen Z, wakati wenyewe wamesema hawana kiongozi wala mwakilishi, Bi Agara anasema: Ruto anaposema anataka kukutana nao nawao wanazidi kupaza sauti wakisema hawana viongizi na hawataki kiongozi inamaanisha anawasikia lakini hataki kusikilizwa wanachosema.

Kulingana naye mambo ya kuanda kungamano la pamoja linalojumuisha washika dau mbali mbali hayatafaulu kwasababu Gen Z wanasema wamewasilisha matakwa yao na kwamba muda umewadia wa kutekeleza masharti hayo kama wanavyotarajia na wala sio maneno matupu.

Rais afanye nini kusitisha maandamano?

Baada ya maandamano makubwa ya juma lililopita ambapo baadhi ya vijana walivamia bunge la taifa Rais alihutubia taifa.

Hutuba hiyo hata hivyo ilizua ghadhabu zaidi badala ya kutuliza hali. Sasa nini kifanyike kusitisha maandamano haya?

Mtaalamu wa masuala ya uongozi Stella Agara anapendekeza rais Ruto:

  • kuwasiliana na familia ya vijana waliouawa katika maandamano na kuwapa pole
  • kufadhili familia zilizoathiriwa ili ziweze kuzika watoto wao
  • kuwaomba vijana hao kutulia ili waliofariki wazikwe kisha waendelee na kazi ya ujenzi wa taifa
Maelezo zaidi:

Imehaririwa na Seif Abdalla